Hali ya ajira nchini katika sekta rasmi kwa mwaka 2012

Utafiti wa Ajira na Mapato (Employment and Earnings Survey) uliofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira wa mwaka 2012 umeonesha kuwa, Sekta rasmi imeendelea kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. Utafiti huo umehusisha masuala mengi yanayohusu ajira, na baadhi ya masuala hayo ni kama ifuatavyo:-
 

 1. Kuna ongezeko la ajira 187,459 (sawa na asilimia 13.8) kwa mwaka 2012 kutoka ajira 1,362,559 mwaka 2011 hadi ajira 1,550,018 mwaka 2012. Utafiti huu umeonesha kuna ongezeko la ajira za masharti ya muda mrefu kutoka ajira 1,102,473 mwaka 2011 hadi kufikia 1,323,733 mwaka 2012. Ajira za muda mfupi zimepungua kutoka 260,086 mwaka 2011 hadi kufikia 226,285 mwaka 2012;  Kupungua kwa ajira za masharti ya muda mfupi kunamaanisha kuongezeka kwa Kazi za Staha, kwani zinakuwa na masuala ya hifadhi ya jamii, likizo, bima za afya n.k.
 2. Utafiti umeonesha kuwa uwiano kati ya ajira za wanawake ukilinganisha na wanaume haukuwa na mabadiliko makubwa kwani wanawake ni asilimia 37.6 mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 37.7 kwa mwaka 2011.
 3. Utafiti unaonyesha kuwa, kati ya ajira 1,550,018 zilizokuwepo katika mwaka 2011/12, kulikuwa na vijana wenye umri wa miaka 15-24 wapatao 37,972 waliokuwa kwenye ajira. Hii ni sawa na asilimia 2.5 ya ajira zote. Aidha, uwiano kati ya ajira kwa vijana wa kike na wakiume haukutofautiana sana. Walikuwepo vijana wa kiume 19,427 na wa kike 18,545 ambao ni sawa na asilimia 1.3 na 1.2 kwa mtiriko huo. 
 4. Utafiti unaonesha kuwa sekta binafsi ndiyo iliyoajiri zaidi ikilinganishwa na sekta ya umma ambapo Sekta binafsi imeajiri asilimia 64.2 na sekta ya umma asilimia 35.8. Hii inaonesha kuwa sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu, serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika miundombinu ya barabara, mawasiliano, nishati n.k ili kuwezesha uwekezaji wa sekta binafsi na kukuza ajira.
 5. Mkoa wa Dar es salaam unaongoza katika kuajiri watu wengi katika sekta rasmi ambapo jumla ya watu 511,596 (sawa na asilimia 33) kati ya watu 1,550,018 wameajiriwa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Ikifuatiwa na Mkoa wa Morogoro ambapo wameajiriwa watu 141,416 (sawa na aslimia 9.1) na Mkoa wa mwisho kwa kuajiri watu ni Rukwa wenye jumla ya ajira rasmi 17,557 (sawa na asilimia 1.1).
 6. Sekta zilizoongoza katika ongezeko la ajira ni elimu, utengenezaji wa bidhaa na usindikaji viwandani na afya; ambapo ajira katika sekta ya elimu imeongezeka kwa asilimia 64.7 kutoka ajira 154,528 mwaka 2011 hadi kufikia 254,538 mwaka 2012, wakati ajira viwandani zimeongezeka kutoka 188,403 mwaka 2011 hadi 260,974 mwaka 2012 sawa na asilimia 38.5. Aidha, ajira kwenye sekta ya afya na ustawi wa jamii imeongezeka kwa asilimia 34.5 kutoka 76,820 mwaka 2011 hadi 103,327 mwaka 2012.
 7. Utafiti unaonesha kuwa sekta ya fedha na bima inaongoza kwa kulipa wastani wa viwango vya juu vya mishahara ambapo kuna wastani wa Tshs. 1,148,299 kwa mwezi kwa mwaka 2012 kutoka Tshs. 834,209 mwaka 2011. Sekta inayofuatia ni ya mawasiliano ambapo inalipa wastani wa TShs. 811,781
 8. Aidha, utafiti unaonesha kuwa watu wengi katika sekta rasmi (zaidi ya asilimia 27) wanalipwa kati ya Tshs. 150,001 na 300,000; wakifuatiwa na wanaolipwa kati ya Tshs. 65,000 na 150,000 (asilimia 22.7). Watu wachache (asilimia 3.9) wanalipwa chini ya Tshs. 65,000 na karibu asilimia 22 wanalipwa kati ya Tshs. 500,001 hadi 1,500,000 kwa mwezi. Hali hii inaonesha kuwa, kwa kiwango kikubwa viwango vya chini vya mishahara vimezingatiwa kwa mwaka 2012.

 
2. Ajira Mpya zilizozalishwa katika Sekta Rasmi katika mwaka wa fedha 2011/12
Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 ajira mpya zilizopatikana katika sekta rasmi ni 74,474 (wanaume 45,835 na wanawake 28,639) kama ilivyochambuliwa hapa chini:-
 

 1. Idadi kubwa ya ajira mpya wameajiriwa watu wa kada za Mafundi na wataalamu washiriki (Technicians and Associate Professionals) watu 31,191 sawa na asilimia 41.9; ikifuatiwa na huduma (Service Workers) ajira 19,594 sawa na asilimia 26.3, Wataalamu (Professionals) ajira 12,134 sawa na asilimia 16.3, Waendeshaji wa mashine na waunganishaji wa mitambo Migodini na Viwandani 2,660 sawa na asilimia 3.6, Kazi zisizohitaji ujuzi 2,575 sawa na asilimia 3.5, Makarani (Clerks) 2,397 sawa na asilimia 3.2 na kada nyinginezo ajira 3,923 sawa na asilimia 5.3
 2. Sekta ya Elimu iliongoza kwa kuajiri idadi kubwa ya wafanyakazi wapya katika kipindi cha mwaka 2011/12  19,745, sawa na asilimia 26.5, ikifuatiwa na Utengenezaji wa bidhaa na usindikaji viwandani 16,703 (asilimia 22.4) , Utawala wa Umma, ulinzi na usalama 12,431 (asilimia 16.7), Afya na Ustawi wa Jamii 7,970 (asilimia 10.7) na Hoteli na migahawa 5,542 (asilimia 7.4).
 3. Mkoa wa Mwanza umeongoza kwa kuzalisha ajira mpya katika mwaka wa fedha 2011/2012 katika sekta rasmi ambapo jumla ya ajira mpya 15,111 (asilimia 20.3) zilipatikana ikifuatiwa na Dar es Salaam ajira 14,158 (asilimia 19.0), Mbeya ajira 5,372 (asilimia 5.4) Shinyanga 3,987 (asilimia 5.4), Kilimanjaro 3,880 (asilimia 5.2), na Mkoa wa Singida ndiyo uliyozalisha ajira chache kuliko mikoa yote ambapo wameajiriwa watu 246 (asilimia 0.3) ya ajira zote.
 4. Utafiti unaonesha kwamba, kati ya waajiriwa wapya; asilimia 30.4 wameanza na mshahara wa kati ya Tshs.65,000 na 150,000, ikifuatiwa na asilimia 30.1 walioanza na mshahara wa kati ya Tshs. 150,001na 300,000, asilimia 36.4 walianza na mshahara wa  zaidi ya Tshs.300,000 na asilimia 3.1 walianza na mshahara wa chini ya Tshs.65,000. Bado tunatoa wito kwa Waajiri kuendelea kuboresha hali bora za wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na maslahi bora kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
 5. Utafiti unaonyesha kuwa, viwango vya mishahara vya kuaniza katika Sekta ya Umma ni vikubwa zaidi vikilinganishwa na Sekta binafsi. Asilimia 16.1 ya watu walioajiriwa mwaka 2011/12 katika Sekta ya Umma walianza na mshahara kati ya TShs.150,001 na TShs. 300,000 wakati asilimia 29.7 ya walioajiriwa katika sekta binafsi walianza na mshahara wa kati ya TShs.65,000 na TShs.150,000. Kwa upande mwingine, kulikuwa na wafanyakazi wachache (asilimia 0.5) katika Sekta ya Umma walioanza na mshahara chini ya TShs. 65,000 ikilinganishwa na asilimia 2.6 katika Sekta Binafsi. Kwa ujumla, watu wengi (asilimia 31.1) walioajiriwa katika Sekta ya Umma walianza na mshahara kati ya TShs. 150,001 na TShs.500,000 na kwa upande wa Sekta binafsi watu wengi (asilimia 43.7) walioajiriwa walianza na mshahara wa kati ya TShs. 65,000 na TShs.300,000.

 
3. Nafasi za Ajira zilizokuwa wazi katika Sekta Rasmi
 

 1. Utafiti umeonesha kuwa katika mwaka wa 2011/12 kulikuwa na nafasi za ajira zilizokuwa wazi 126,073. Kati ya nafasi hizo, asilimia 76 hazikuhitaji uzoefu wowote; asilimia 17.3 zilihitaji uzoefu wa mwaka 1 hadi 2, asilimia 5.9 zilihitaji uzoefu wa miaka 3 hadi 4 na asilimia 0.7 tu ndizo zilizohitaji uzoefu wa zaidi ya miaka 5.
 2. Nafasi za kazi zilizokuwa wazi zilihitaji zaidi watu wenye ujuzi katika maeneo yafuatayo: watu wenye ujuzi katika masuala ya Elimu zilikuwa nafasi 54,828 (asilimia 43.5); Utawala wa Umma na Ulinzi 36,531 (asilimia 29.0); Afya watu 19,053 (asilimia 15.1); Utaalamu, sayansi na ufundi 4,358 (asilimia 3.5), Hoteli na migahawa 2,670 (asilimia 2.1); Kilimo 2,597 (asilimia 2.1) na huduma nyinginezo 1,537 (asilimia 1.2).
 3. Asilimia 83.9 ya nafasi za kazi zilizokuwa wazi hazikutaja zinahitaji mtu wa jinsi gani; asilimia 9.5 zilihitaji mwombaji awe mwanaume na asilimia 6.5 ya nafasi zote zilihitaji mwombaji awe mwanamke.  

 
4. Hitimisho
Matokeo haya yanaashiria mambo yafuatayo:

 1. Idadi kubwa ya waajiriwa kuwa katika masharti ya muda mrefu kuna ashiria kuimarika kwa ajira zenye staha; ambapo masuala ya hifadhi ya jamii, bima ya afya na likizo yanazingatiwa.
 2. Uwiano kati ya wanawake na wanaume unaendelea kuwa mzuri ambapo kwa mwaka 2012 kati ya ajira zote wanawake ni asilimia 37.6
 3. Matokeo yanaonesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uhamaji nguvu kazi (Labour Migration) kutoka kutoka Mikoa mingine na kuhamia Dar es Salaam; ambapo asilimia 33 ya waajiriwa wote wa sekta rasmi wapo Dar es Salaam. Natoa rai kwa wawekezaji kuwekeza zaidi Mikoa mingine ili kuweza kutoa fursa za ajira katika sekta rasmi.
 4. Suala la upatikanaji wa Takwimu za ajira lina changamoto kubwa kutokana na kwamba waajiri wengi hawapendi kutoa taarifa japokuwa sheria inawataka kufanya hivyo.  Ili serikali iweze kupanga matumizi mazuri ya nguvu kazi nchini suala la upatikanaji wa taarifa za soko la ajira halikwepeki. Hivyo natoa rai kwa waajiri wote kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Kazi na Ajira na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kutoa taarifa sahihi kuhusu ajira katika maeneo yao ya kazi.